What's New

Welcome To the THTU Homepage My Files What's New Contact THTU Members My Photos

THTU News

 

TAARIFA KWA UMMA NA VIONGOZI WA SERIKALI JUU YA

MSIMAMO WA THTU KUHUSIANA NA MGOGORO WA TAASISI YA USTAWI WA JAMII

25 Agosti 2011

DAR  ES SALAAM

 

Wanachama na uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (THTU) wamepokea kwa masikitiko makubwa kupitia vyombo vya habari vya hapa nchini hatua ya Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW) kusitisha  mara moja ajira za wahadhiri wapatao 21 kuanzia tarehe 17 Agosti, 2011 kwa kisingizio cha kuendesha mgomo usio halali na kukaidi maagizo ya mamlaka za juu. Chama cha THTU ngazi ya Tawi na Taifa kimefuatilia mgogoro wa ISW uliosababishwa na Menejimenti na Bodi ya Magavana wa Taasisi kushindwa kutekeleza maagizo halali ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) tangu Mwaka 2007. Chama kimepitia pia andiko lililopelekwa na Menejimenti ya ISW kwa Bodi ya Magavana ili Bodi iwachukulie hatua za kinidhamu wahadhiri hao 21. Chama cha THTU kikizingatia mawasiliano mbali mbali baina ya NACTE na Uongozi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii na mawasiliano baina ya uongozi wa wanataaluma na pia uongozi wa THTU tawi la Taasisi ya Ustawi wa Jamii na Menejimenti, Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana, Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (Wizara mama ya Taasisi) na Waziri Mkuu,  kinapenda sasa kutoa tamko kwa umma wa Tanzania, Uongozi wa Taasisi husika na Viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Tanzania.

 Andiko la Bodi ya Magavana wa Taasisi iliyowafukuza wahadhiri 21 linadai yafuatayo: 
  1. Taaasisi ya Ustawi wa Jamii imekumbwa na mgomo wa kikundi cha wahadhiri ishirini na mmoja (21) tangu tarehe 28 June, 2011 hadi leo.
  2. Mgomo huu ulisababisha shughuli zote za mafunzo na usimamiaji wa mafunzo kwa vitendo, tafiti za wanafunzi na kazi zote za mwajiri kusimamishwa jambo hili lilisababisha hasara kubwa kwa mwajiri.
  3. Kutokana na mgomo huo Taasisi ilisitisha masomo tarehe 21 Julai 2011.
  4. Mbinu zote za muafaka na kikundi hiki cha wahadhiri zilishindikana.
  5. Mbinu hizo ni pamoja na Menejimenti, kuwasihi kuendelea kufanya kazi na kuchukua barua za kujieleza na kuja kwa ajili ya utatuzi wa mgogoro
  6. Mwenyekiti wa Bodi na Makamu wake waliwasihi wote kuacha tendo hilo.
  7. Vile vile Mwenyekiti na Bodi yake waliongea na wahadhiri hao na kuwasihi wachukue barua na wakakaidi hadi leo hii isipokuwa Mwalimu mmoja tu ambaye atakuja mbele ya Bodi kwa mahojiano
 Ukweli kuhusu kiini cha mgogoro wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii ni huu hapa: 
  1. Barua za NACTE zenye kumbukumbu NACTE/DA/31/655/Vol.I/92 ya tarehe 19 Juni 2007; NACTE/DA/309/669/Vol.I/27 ya tarehe 15/7/2010; na NACTE/CA/28/67/5/Vol.XI/34 ya tarehe 19/8/2010; zinaonyesha Taasisi ya Ustawi wa Jamii ilipewa maagizo ya kufanya maboresho ili kukidhi matakwa ya ithibati yanayokubalika  NACTE na Taasisi ilipokaidi maagizo ya NACTE ilizuiliwa kujihusisha na udahili wa programu za ngazi ya cheti, stashahada na shahada (certificate, diploma and degree programmes) ilipofika Aprili 2011.
 
  1. Maagizo ya NACTE kwa Taasisi yaliweka bayana kuwa Taasisi ilizuiliwa kudahili kwa kuwa ilishindwa kukidhi matakwa ya ithibati ya kwanza iliyoidhinishwa na NACTE kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2006 hadi Machi 2011. Kwa barua hizo Taasisi ilipewa muda mpya wa kuandaa mitaala na kurekebisha mfumo wa utawala hadi ifikapo Septemba 2011 ili warudishiwe haki ya kuendesha programu.
 
  1. Maagizo ya NACTE yaliweka bayana pia kuwa Taasisi ilizuiliwa kuendesha programu hizo kwa kuwa haikuwa na mfumo wa utawala unaokubalika chini ya sheria ya NACTE kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya cheti, stashahada na shahada kwa mujibu wa Sheria ya NACTE.
 

Wanataaluma wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii walifanya jitihada mbalimbali kuanzia mwaka 2008 kuisihi Menejimenti, Bodi ya Magavana na Serikali kufanya marekebisho yaliyohitajiwa na NACTE bila kusikilizwa na badala yake Menejimenti iliwaona wakorofi. Haja ya msukumo kutoka kwa wanataaluma ilitokana na Taasisi kufutiwa Programu ya Menejimenti ya Rasilimali Watu.  Viongozi wa wanataaluma na chama cha wafanyakazi walifikisha tatizo la ISW kufutiwa programu kwa Mh Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii.  Pamoja na maelezo mazuri na ahadi nzuri zilizotolewa katika kikao na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kilichofanyika tarehe 25 Julai 2011, wahadhiri waliokuwa waliokuwa kwenye kikao hich waliporejea Chuoni Menejimenti ikafunga mageti ili kuwalazimisha kichukua barua za kusimamishwa kazi. Jambo hili liliashiria dhahiri kuwa Katibu Mkuu hakuwa na nia ya kutatua mgogoro huo bali aliwatoa Chuoni ili kuipa nafasi Menejimenti kujipanga dhidi yao na hii ni hadaa mbaya kufanyiwa watu wazima wenye dhamana ya kutoa taaluma. Wahadhiri waliomba pia kukutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana Prof. Msambichaka lakini hakuweza kutoa maelezo muafaka ya kurejesha Taasisi katika hadhi yake inayoporomoka, bali akashinikiza tu wapokee barua ambazo hazikutolewa kwa mujibu wa Taratibu za Ajira za Taasisi (Staff Regulations) na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya 2004.

 

Baada ya viongozi wa wanataaluma na chama cha wafanyakazi kuona udhalimu unataka kufanyika dhidi ya wahadhiri na taasisi yao waliuwasilisha mgogoro huo katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na wakapewa tarehe ya kufika kwa majadiliano. Lakini pamoja na kupokea wito wa kuitwa kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (rejea wito Na. CMA/DSM/KIN/558/11) kwa ajili ya majadiliano tarehe 29/7/2011 na tarehe 15/8/2011, Menejimenti na Bodi ya Magavana ilikaidi na kuharakisha kukifanya kile walichokitaka wao kwa kuwafukuza wahadhiri 21 ili wafunike udhaifu ulioko ndani ya uongozi wa Taasisi na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

  Tamko la THTU: 

Kwa sababu zilizoainishwa ndani ya waraka huu Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (THTU) kinatoa tamko lake kama ifuatavyo:

 
  1. Si kweli kuwa wahadhiri walioachishwa kazi walifanya mgomo usio halali. Ikumbukwe kwamba kunako Aprili 2011 Taasisi ilizuiliwa na NACTE kudahili wanafunzi kwa ajili ya kozi za cheti, stashahada na shahada hivyo ilikuwa ni sahihi kufanya vikao vya wanataaluma ili kujadili hatima ya Taasisi yao. Aidha inashangaza  kuona kwamba baadhi ya wahadhiri waliosimamishwa kazi walikuwa na ruhusa halali walizopewa na mwajiri kama likizo za kufanya mitihani ya vyuo vingine wanakosoma kama Mzumbe, wengine walikuwa safarini kwa ajili ya matatizo ya kifamilia na mengineyo.

  1. Dai la Bodi ya Magavana kuwa wahadhiri 21 walisababisha hasara halina mantiki kwani tayari hasara hiyo ilishapatikana tangu Bodi ya Magavana na Menejimenti waliposhindwa kutekeleza maagizo halali ya NACTE.
 
  1. Maamuzi ya Bodi ya Magavana kuwasimamisha kazi wahadhiri 21 kwa kisingizio kwamba walifanya mgomo usio halali yalilenga kulinda mapungufu ya kiutendaji yaliyo dhahiri yaliyofanywa na menejimeji dhaifu na Bodi isiyo makini.
 
  1. Andiko lililopelekwa na menejimenti kwa Bodi ya Magavana wa Taasisi lilipelekwa kwa namna ya kukiuka Kanuni za Ajira  za Taasisi ya Ustawi wa Jamii (Staff Regulations) na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya 2004.
 
  1. Menejimenti ya Taasisi imekiuka haki za msingi za wafanyakazi walioachishwa kazi bila kufuata Kanuni za Taasisi ya Ustawi wa Jamii; Sheria ya Kazi Na 6 ya mwaka 2004 na kwa mujibu wa Katiba ya Nchi.
 
  1. Menejimenti ya Taasisi imewadhalilisha wahadhiri walioachishwa kazi wakiwa wanatetea maslahi ya Taasisi, maslahi ya wanafunzi wa Taasisi na maslahi ya Umma mzima wa Tanzania kwa kuwafukuza kwa njia ya Magazeti, Radio na Televisheni. Chama cha THTU kinalaani vikali hatua hiyo ya Bodi kutumia rasilimali haba za Taasisi kuwadhalilisha watetezi wa Taasisi!
 
  1. Kutokana na hali hii, Chama cha THTU kina haki ya kuchukua hatua mbalimbali kuzuia udhalimu huu mkubwa dhidi ya wahadhiri hao 21 na Taifa letu kwa ujumla usifanikiwe  ikiwa ni pamoja na kuishitaki Menejimenti ya Taasisi mbele ya Umma na Mahakamani na pia kuishitaki Serikali kwa Wananchi wake  kwa kushindwa kuyafanyia kazi maagizo yaliyotolewa na chombo chake chenye mamlaka ya kuongoza taasisi kama ISW, yaani NACTE.
 
  1. Chama cha THTU kimesikitishwa na Bodi ya Magavana kutofanyia kazi makubaliano ya kikao cha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na wahadhiri cha tarehe 25/7/2011 na badala yake Bodi ilifanya maamuzi ya kuwaachisha kazi wahadhiri 21 wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii.

  1. Chama kinaamini kuwa hatua ya Menejimenti, Bodi ya Magavana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kufanya udhalimu huu wa wazi inaashiria kuwa pana matatizo makubwa yanayoigubika Taasisi ya Ustawi wa Jamii na yanayolindwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii hali inayopelekea maamuzi yasiyo na mantiki wala tija kwa nchi yachukuliwe dhidi ya wahadhiri wanaotetea hadhi ya Taasisi.
 
  1. Chama cha THTU kimesikitishwa na upotoshwaji uliofanywa na Mhe. Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii alipoudanganya umma kupitia Bunge tarehe 12 Julai 2011 kwamba hali ya Taasisi imeboreshwa baada ya kuwa na uongozi mpya katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii wakati kuanzia mwezi Aprili 2011 Taasisi ilikatazwa kudahili wanafunzi katika mwaka mpya wa masomo kwa sababu ya kutokukidhi matakwa ya ithibati pamoja na kuwa na menejiment isiyokuwa na sifa stahiki.
 
  1. Chama kinatoa wito kwa matawi yote ya THTU nchini na pia kwa vyama vingine vya wafanyakazi katika taasisi za Elimu ya Juu kujadili mgogoro wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii kwa kina na kuutolea maamuzi na matamko ya kuutetea msimamo wa NACTE na wahadhiri waliofukuzwa bila kufuata taratibu.
 
  1. Chama cha THTU ngazi ya Taifa kinaupongeza uongozi wa NACTE kwa kuwa makini kusimamia mitaala katika Taasisi za Elimu ya Juu na kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata elimu bora na sahihi kama ilivyofanyika kwenye Taasisi ya Ustawi wa Jamii.
 
  1. Mwisho, Uongozi wa THTU unaishauri Serikali ifanye hima kuchunguza kwa dhati mgogoro wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii na kutoa maamuzi ya haki dhidi ya wahadhiri wote  na wafanyakazi waliofukuzwa na kuiimarisha Taasisi kama ilvyopendekezwa katika barua ya wanataaluma wa Taasisi za Ustawi wa Jamii kwa Mh Waziri Mkuu ili Taasisi iweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria ya NACTE.
 Taasisi ya Ustawi wa Jamii iwaombe radhi wahadhiri wote waliofukuzwa kazi na kuwarudisha haraka kazini bila masharti kwa sababu taratibu hazikufuatwa. NIA NA MWELEKEO WETU DAIMA NI KUJENGA“TAIFA KWANZA”  

 Kulu S. Maswanya

Kaimu Katibu Mkuu THTU Taifa

 

MKUTANO          MKUTANO           MKUTANO

TAARIFA YA MKUTANO KWA WANACHAMA NA WAFANYAKAZI WA TAASISI ZA ELIMU YA JUU TANZANIA

KUTAKUWA NA MKUTANO WA WANACHAMA NA WAFANYAKAZI WA TAASISI ZA ELIMU YA JUU TANZANIA SIKU YA JUMAMOSI TAREHE 29/01/2011 KUANZIA SAA 09:00 ASUBUHI KATIKA UKUMBI WA NKURUMAH.

WOTE MNAKARIBISHWA.

NIA NA MWELEKEO WETU DAIMA NI KUJENGA. 

UCHAGUZI WA MATAWI ULIOFANYIKA SIKU ZA KARIBUNI

Chama bado kinaendelea na mchakato wake wa kutembelea Vyuo mbalimbali na siku ya hivi karibuni Vyuo kadhaa viliweza kufanya uchaguzi wa Matawi, navyo ni:- 

Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE)

Tarehe ya Uchaguzi 29/10/2010 

Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW)

Tarehe ya Uchaguzi 24/11/2010

Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU)

Tarehe ya Uchaguzi  30/12/2010

Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM)

Tarehe ya uchaguzi  21/01/2011

National Workers Conference

The THTU national meeting recived and approved the following themes for the proposed National Workers Conference to be held on the 29-30 April 2010 the week before the May Day celebrations:

  1. Hali ya Wafanyakazi na Harakati za Vyama vya Wafanyakazi kabla na baada ya Uhuru (Struggles by Workers Unions for Improved Working Conditions and Earnings Before and After Uhuru)
  2. Mazingira ya Kazi na Usalama kwa Afya za Wafanyakazi katika Mazingira ya Mfumo wa Uchumi Huria/ Kandamizi (Working Conditions and Workers Safety Under the Globalised Economy)
  3. Umuhimu wa kuwa na mfumo bora na imara wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (The importance of a good, stable and functioning Public Social Security System)
  4. Ushiriki wa akina Mama katika harakati za Wafanyakazi (The Role of Women in the Workers Struggles)
  5. Umuhimu wa Ushiriki wa Tabaka la Wafanyakazi katika Siasa na maendeleo ya Nchi (The Improtance of Workers Participation in the Political Process in National Development)
  6. WOMENS DAY - 15 YEARS AFTER BEIJIN

    THTU Kamati ya Wanawake, ilishiriki kikamilifu katika siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa tarehe 08/03/2010.

    Kitaifa THTU Kamati ya Wanawake ilipeleka wawakilishi wawili mkoani Tabora ambapo maadhimisho hayo yalifanyika Kitaifa,Wawakilishi hao ni Mwenyekiti wa Wanawake MUHAS Bi. Rose B.E. Mtui na Kaimu Mwenyekiti wa Wanawake UDSM Bi. Magreth Bwathond. Wawakilishi hao pia walipata nafasi kukutana na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa akiwemo Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo.

    THTU Kamati ya Wanawake, iliadhimisha siku hiyo Kimkoa hapa Dar es salaa katika viwanja vya Mnazi Mmoja. Katika maadhimisho hayo Kamati za Wanawake ziliwakilishwa na Matawi yafuatayo:- Chuo Kikuu Ardhi (ARU), Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS), Chuo Kikuu Cha Dar es salaam (UDSM), Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es salaam (DUCE), Chuo Cha Ustawi wa Jamii (ISW), Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania (OUT) na Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE).

     

     


    BROWSE OLD POSTS